Guarding and proclaiming the unchanging truth in a changing world

Waraka kwa makania mkutano wa Gafcon 2018

“Mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”  (Matendo 1:8)
 

Salamu kutoka nchi ya kuzaliwa, huduma, kifo, ufufuo na kupaa kwa Bwana wetu wa  utukufu Yesu Kristo. Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Anglikana Ijayo (Gafcon) ulifanyika Yerusalemu mnamo mwezi wa Juni 2018, miaka kumi baada ya Gafcon kuanzishwa mwaka 2008. Gafcon 2018, mojawapo ya mikutano mikubwa ya Waanglikana duniani, iliwakusanya  wawakilishi 1,950 kutoka nchi 50, ikiwa ni pamoja na maaskofu 316, wachungaji 669  na walei 965. Umoja wa roho ulionekana katika Mkutano huo ambapo tulikutana na Mungu mbele ya marafiki kutoka maeneo mbalimbali. Tulifanya ibada kwa furaha, kushiriki katika maombi kwenye vikundi vidogo vidogo  na tulitiwa moyo kwa hotuba, mikutano ya vikundi na semina.
 
Tulikutana pamoja tukiongozwa na mada kuu "Kumtangaza Kristo kwa Uaminifu kwa Mataifa". Kila siku ilianza na ibada ya kawaida na mafundisho ya Biblia kutoka Injili ya Luka 22-24, ikifuatiwa na  vipindi maalum juu ya Injili ya Mungu, Kanisa la Mungu na Dunia ya Mungu.

KUTANGAZA INJILI YA MUNGU

Tuliuisha upya nia yetu ya kutangaza Injili ya Mungu wa Utatu katika makanisa yetu na ulimwenguni kote. Mwenyekiti wetu alitukumbusha kwenye hotuba yake ya ufunguzi kwamba: "Injili ya Mungu ni ujumbe wa wokovu unaobadilisha maisha ya mtu kutoka kwenye dhambi na matokeo yake kwa njia ya kifo na ufufuo wa Bwana Yesu Kristo. Huu ni mwitikio wa kukubali lakini pia ni agizo: injili inatutangazia kile kilichofanyika kwetu katika Kristo pia kututaka kutubu, kuwa na imani na kuwa na utii katika Bwana." Injili inahusisha kurejeshwa na kuthibitisha makusudi ya uumbaji wa Mungu. Injili ni kwa ajili ya wanaume, wanawake na watoto na ndio matumaini yetu pekee wakati  wa hukumu ya mwisho na uhalisia wa kuzimu.

Hii ni injili ya Mungu, injili inayomhusu Mwana wake (Warumi 1:1-3). Kiini cha ujumbe wa injili ni huyu mtu mmoja, Yesu Kristo, na yote aliyoyafanya kupitia maisha yake makamilifu, kifo cha upatanisho, ufufuo wa ushindi na kupaa kwa utukufu. Kila siku katika mafundisho yetu ya biblia, tulifuata njia ya Yesu kuanzia kwenye hukumu ya Pilato na viongozi wa Kiyahudi, mpaka kwenye kifo chake kwa ajili yetu pale msalabani, mpaka alipovunja vifungo vya kifo siku ya asubuhi ya Pasaka na mpaka kuwaagiza wanafunzi wake kutangaza "toba ya msamaha wa dhambi kwa njia ya jina lake kwa mataifa yote "(Luka 24:47). Upekee wa Yesu Kristo  ndio kiini cha Injili: "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo" (Matendo 4:12). Injili inakutana nasi tukiwa  katikati ya kuchanganyikiwa na dhambi zetu lakini haituachii hapo. Inatuelekeza kwenye toba na kutuita kuiamini injili (Marko 1:15), ambayo inaleta maisha yaliyojaa neema. Kristo aliyepaa kwenda mbinguni aliwapa wanafunzi wake Roho wake ili kuwawezesha kupeleka hii injili  ulimwengu kote.

Hata hivyo, kutangaza kwa uaminifu injili hii  kumekuwa chini ya mashambulio kutoka nje na ndani, kama ilivyokuwa  wakati ule wa mitume (Matendo 20:28-30).

Mashambulio ya nje yanajumuisha tamaduni na imani potofu za kutoa kafara ambazo zinapinga utoshelevu wa sadaka ya Kristo aliyoitoa mara moja. Baadhi ya dini zinakana upekee wa maisha na kazi za Yesu Kristo msalabani, na wengine wanachanganya injili na imani potofu. Imani ya kutohusisha dini kwenye jamii (Secularism) hutafuta kumtenga Mungu kutoka kwenye majadiliano yote ya umma na kuvunja urithi wa Kikristo wa mataifa mengi. Hii imekuwa wazi zaidi katika mafafanuzi mapya yanayoelezea nini maana ya kuwa binadamu, hasa katika maeneo ya jinsi, jinsia na ndoa. Kutokumthamini binadamu kwa kutetea utoaji mimba na kusaidiwa kujiua pia ni shambulio juu ya maisha ya mwanadamu aliyeumbwa kipekee kwa mfano wa Mungu. Kuna makundi ya kidini na wafuasi wa imani ya kutohusisha dini kwenye jamii wenye chuki dhidi ya kuhubiri Injili  na wanawatesa wanaohubiri Kristo.

Kwa mashambulio ya ndani, "injili ya mafanikio" na utafutaji wa tafsiri mpya za kitheolojia, zote zinatafuta njia mbalimbali za kuelezea Injili ya Mungu kwa kupokea tamaduni zinaozowazunguka, na kusababisha kuchanganya injili na utamaduni ambao hupotosha upekee wa Kristo, madhara ya dhambi, haja ya kutubu na mamlaka ya mwisho ya Biblia.
 
Kwa masikitiko makubwa, kumekuwa na kushindwa kwa uongozi wa makanisa yetu kushughulikia mambo haya yanayoshambulia injili ya Mungu. Tunatubu kushindwa kwetu kuzingatia maneno ya mtume Paulo: "jilindeni nafsi zenu, na mlinde kundi lote la kondoo ambalo Roho Mtakatifu ameliweka chini ya uongozi wenu; mtunze kanisa la Mungu ambalo amelinunua kwa damu ya Mwanae. Najua kwamba nikishaondoka, mbwa mwitu wakali watakuja kati yenu nao hawatakuwa na huruma yo yote juu ya kundi lenu. Na hata kati yenu ninyi patatokea watu watakaosema maneno ya kupotosha ili wawavute baadhi ya wanafunzi wawafuate."(Matendo 20:28-30).
 
Tunajitia wakfu upya kumtangaza Kristo kwa uaminifu kwa mataifa, tukifanya kazi kwa pamoja  kulinda Injili tuliyopewa na Bwana wetu na mitume wake.

KUFANYIA MATENGENEZO KANISA LA MUNGU

Injili ya Mungu huunda kanisa la Mungu. Kupitia mwaliko wa injili, Mungu anawaita watu wote katika ushirika wa Mwanawe, Bwana Yesu Kristo. Kwa kuwa neno la injili huwafikia watu kwa nguvu za Roho Mtakatifu, watu hupokea neno kwa njia ya Roho Mtakatifu kwa kutubu, kuamini na kubatizwa, na hivyo hujiunga na mwili wa Kristo ambao ni kanisa lake (Matendo 2:37-44; 1 Wakorintho 12:12-13). Kama viungo vya mwili wa Kristo, wanatakaswa katika yeye, wanaitwa kuishi maisha ya utakatifu na kuwa chumvi na nuru ya dunia.
 
Mkutubi mmoja katika Mkutano alitukumbusha hivi: "Katika mabaraza ya kanisa, tusiige mambo ya dunia bali tukusanyike ili kuomba, kusifu (yaani, ushirika mtakatifu), kushauriana, kufanya maamuzi, na kama ikilazimu kurekebishana nidhamu. Mikusanyiko hii inatakiwa kuwa ya upatanisho wa kama baraza kwa asili, na kuweza kufanya maamuzi ya kulipeleka kanisa mbele katika utume na maisha yake. Kuna haja ya kuchukua hatua za kinidhamu kwa upendo lakini pia kuwa na msimamo mkali ili kuwafanya wenye dhambi watubu na kurejeshwa kundini. Vivyo hivyo katika ngazi ya Jumuiya ya Waanglikana Duniani, kuna wakati ambapo uongozi unapaswa kuchukua hatua za pamoja kutekeleza jukumu lake la kuadhibu jimbo lililokosea.
 
Kwa muda sasa, Jumuiya yetu ya Kimataifa imekuwa kwenye tishio kutoka kwa viongozi wanaokataa Utawala wa Kristo na mamlaka ya Maandiko. Mwishoni mwa karne ya 20, ujinsia wa binadamu umekuwa suala linalosumbua.
 
Mkutano wa Lambeth 1998, kwa idadi ya kura nyingi (526 kwa 70) ulipitisha Azimio I.10 juu ya Ujinsia wa Binadamu, ambao umethibitisha mafundisho ya Yesu katika Mathayo 19 kwamba kuna aina mbili tu za uaminifu wa matumizi ya jinsia: ndoa ya kudumu kati ya mwanamume na mwanamke au kujizuia. Azimio hilo lilitaka kuwepo kwa huduma ya kichungaji kwa watu wanaovutiwa na mapenzi ya ngono ya  jinsia moja.  Wakati huo huo, azimio hilo lilielezea vitendo vya ushoga kuwa  "havikubaliani na Maandiko" na kukataa idhini zote za ibada za ndoa za jinsia moja ndani ya Kanisa na kutokuwaamuru wote  walio katika mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja.

Azimio la Lambeth I.10 lilionyesha kuongezeka kwa ushawishi mkubwa wa Nyanda za Kusini za Dunia katika Jumuiya ya Waanglikana Kimataifa. Msingi wa Azimio hili uliandaliwa na Taarifa ya Kuala Lumpur ya 1997 ya Mtandao wa Waanglikana wa Nyanda za Kusini za Dunia. Ushirikiano wetu na Mtandao wa Nyanda za Kusini za Dunia umekuwa unaendelea, na viongozi wake walishiriki kikamilifu katika Mkutano huu wa Lambeth.

Kukataliwa kwa Azimio la Lambeth I.10 kwa maneno na kwa matendo na Kanisa la Anglikana Marekani (Episcopal USA) na baadaye na majimbo mengine ya Kianglikana kulisababisha “kuchanika kwa kitambaa cha Jumuiya kwa kina sana”,  kufuatiwa na miaka kumi ya mikutano isiyokuwa na tija ambapo Mihimili minne vya Jumuiya haikufanikiwa kuchukua hatua stahiki za kinidhamu. Kikao cha Maaskofu Wakuu pia kiliyataka majimbo haya kutubu na kuirudia imani. Hata hivyo jitihada zao zilishushwa chini na Mihimili mingine ya Jumuiya, hasa kushindwa kwa Ofisi ya Askofu Mkuu wa Canterbury kutekeleza makubaliano ya wazi ya Kikao cha Maaskofu Wakuu kilichokutana huko Dar es Salaam mwaka 2007.

Katika Taarifa na Azimio la Yerusalem, Mkutano wa Kimataifa wa Anglikana Ijayo (Gafcon) wa 2008 ulikubali kuchukua hatua na changamoto ya kurejesha mamlaka ya kibiblia (hasa juu ya  mafundisho ya ujinsia wa binadamu) kwa kuthibitisha uhalisia wa  Biblia kama Neno la Mungu lililoandikwa na kurudi kwenye vyanzo vingine vya Utambulisho wa Waanglikana – Imani (kama vile Imani ya Nikea) na Halmashauri za kanisa la kwanza, Makala 39, Kitabu cha Sala kwa Watu Wote na taratibu za kuamuru wahudumu cha mwaka1662. Mkutano huo pia ulianzisha Baraza la Maaskofu Wakuu ambao waliidhinisha kutambua makanisa ya Anglikana katika maeneo ambapo Waanglikana wenye kufuata mafundisho ya kweli walikuwa wamepokonywa mali zao za kanisa na kuondolewa kwenye madaraja matakatifu. 

Katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita, Mihimili ya Jumuiya sio tu imeshindwa kuchukua hatua za kinidhamu za kimungu lakini pia wawakilishi wake wamekataa kutambua mtazamo wetu na badala yake wamechagua kuidunisha Gafcon kama kikundi kinachoshinikiza suala moja tu na kuituhumu kwa matengano ilihali wanaosababisha mpasuko ni wale waliokengeuka na kuacha mafundisho ya Biblia pamoja na mafundisho ya kihistoria ya Kanisa. Kauli mbiu kama vile “kutembea pamoja” na “kukubali kutokukubaliana” ni zenye kupotosha kwa hali ya juu na zinalenga kuwashawishi watu kukubali mafundisho potofu katika Jumuiya. 

Tunahuzunishwa na hali ya Jumuiya yetu Duniani kwani imezuiwa kutimiza kusudi lake lililopewa na Mungu la kuwafikia mataifa kwa habari ya Kristo. Tunatubu kutokana na kushindwa kwetu kusimama thabiti katika imani (1 Wakorintho 16:13). Lakini hatupotezi tumaini kwa mambo yajayo, na tunatambua kwamba kuna msaada thabiti kwa ajili ya kuleta matengenezo kwenye Jumuiya yetu. Kabla ya Gafcon 2018, wajumbe, kwa wingi wao waliafiki mapendekezo yafuatayo:

  • Azimio la Lambeth I. 10 linaakisi mafundisho ya Biblia yasiyobadilika;
  • Harakati za Gafcon zingeendeleza uaminifu kwa Azimio la Yerusalemu;
  • Baraza la Maaskoofu Wakuu liendelee kutambua mamlaka za Waanglikana wenye imani ya kweli. 

Zaidi ya miaka ishirini iliyopita tumeuona mkono wa Mungu ukituongoza katika kufanya matengenezo ya Jumuiya ya Waanglikana Duniani. Tangu mwanzo Gafcon imetanabaisha: “Hatuachi Jumuiya ya Waanglikana; Sisi ni wengi ndani ya Jumuiya ya Waanglikana na tunatafuta kuendelea kuwa waaminifu kwa urithi wetu wa Kianglikana.” Kama ambavyo baba Askofu Mkuu Nicholas Okoh alisema katika ufunguzi wa Baraza la Sinodi: “Tunafanya kile ambacho uongozi wa Jumuiya ungefanya kutekeleza azimio lake lenyewe la mwaka 1998.” 

Tunatoa shukrani kwa ajili ya ujasiri wa Kimungu wa Maaskofu Wakuu wa Gafcon katika kutetea imani ambayo ilitolewa mara moja tu kwa watakatifu wote. Tunapongeza maamuzi yao ya kuthibitisha na kutambua maeneo ya Kanisa la Anglikana la Amerika Kaskazini na Kanisa la Anglikana(ACNA) la Brazil, kutambua misheni ya Kanisa Anglikana Uingereza na kumtia wakfu Askofu wa kimishenari wa bara la Ulaya. Jambo hili limekuwa la muhimu kutokana na kuachwa kwa Imani kwa makanisa ya Marekani (Episcopal) Canada (ACC), Brazil (Episcopal) na Scotland (Episcopal). Katika Gafcon ya 2018 tulisikia shuhuda mbalimbali za Waanglikana waaminifu wanaoteswa na wale wanaoshikilia nyadhifa mbalimbali kwenye maeneo yao kwa sababu walikataa kujisalimisha wala kuruhusu kupotoshwa na injili ya uongo ambayo viongozi hao wanakiri na kueneza. Pia tunatambua utayari wa Maaskofu Wakuu wa Gafcon kuwasaidia Waanglikana wenye imani ya kweli wa New Zealand ambapo hivi karibuni Kanisa la Anglikana (New Zealand) liliwaruhusu Maaskofu kuidhinisha baraka kwa mashoga wenye ushirikiano wa jinsia moja.

Kadri harakati za Gafcon zinavyoendelea kuimarika, pamekuwa na uhitaji wa mfumo wa baraza la uongozi. Tunakubaliana na kuundwa kwa Matawi ya Gafcon pale inapohitajika pamoja na Jopo la Washauri linalojumuisha maaskofu, wachungaji na walei kutoka katika kila Jimbo na Tawi la Gafcon ili kushauri Baraza la Maaskofu Wakuu. Pamoja na Maaskofu Wakuu, Jopo la Washauri litaunda Baraza la Sinodi ambalo litaleta mapendekezo kwenye Mkutano wa Gafcon. Baraza la Sinodi lilikutana kwa mara ya kwanza kwenye mkutano huu.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya Baraza la Sinodi, tunamhimiza kwa heshima Askofu Mkuu wa Canterbury:

  • kuwaalika kama wajumbe kamili kwenye Lambeth 2020  maaskofu wa Jimbo la Kanisa la Anglikana la Amerika ya Kaskazini (ACNA) na Kanisa la Anglikana la Brazil na
  • kutowakaribisha maaskofu wa Majimbo ambayo kwa maneno na kwa matendo wamekubali vitendo vya ngono ambavyo viko kinyume na mafundisho ya Maandiko Matakatifu na Azimio  I.10 la Mkutano wa Lambeth wa 1998, isipokuwa kama wametubia matendo yao na kubatilisha maamuzi yao.

Iwapo haya hayatatekelezwa, tunawahimiza wajumbe wa Gafcon  kukataa mwaliko wa kuhudhuria Lambeth 2020 na vikao vingine vyote vya Mihimili ya Jumuiya.

KUWAFIKIA WATU WA MUNGU

Maudhui ya mkutano wetu umekuwa ni “Kumtangaza Kristo kwa Uaminifu kwa Mataifa.” Tumeipokea injili kupitia kwa mashahidi waaminifu wa vizazi vilivyopita. Lakini bado wapo mabilioni ya watu ambao hawajampokea Kristo na hawana tumaini. Yesu aliwafundisha wanafunzi wake: “hii habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote kuwa ushuhuda wa mataifa yote” (Mathayo 24:14)

Tunatubu kwa nyakati na majira ambayo tumekuwa tukijihubiria sisi wenyewe badala ya kubeba jukumu gumu la kuvuka mipaka ya makundi yetu ya asili na kuitikia wito wa Mungu kwamba tuwe nuru ya mataifa (angalia. Matendo 13:47). Kwa imani na utiifu, tunafurahi kujirejeza kwa upya katika kuihubiri injili kwa uaminifu.

Ili kupanua uwezo wetu wa kumtangaza Kristo kwa uaminifu kwa mataifa katika maneno na matendo, tulizindua mitandao tisa ya kimkakati.

Elimu ya kitheolojia - Kukuza ufanisi wa mafunzo ya kitheolojia katika Jumuiya Waanglikana duniani kote
Uanzishaji makanisa mapya - Kupanua mpango wa kufungua makanisa mapya kama mkakati wa kimataifa kwa ajili ya uinjilisti
Ushirika wa kimataifa wa utume - Kukuza ushirika wa utume na utumishi katika ulimwengu huu wa utandawazi
Huduma ya vijana na watoto - Kuwa kichocheo kwa ajili utume wa vijana na watoto wa mataifa yote ili wafanyike wanafunzi watiifu wa Yesu Kristo
Muungano wa wamama - Kupanua uwezo wa huduma hii ya kimataifa ya kukuza mafundisho ya kibibilia kuhusu ndoa na maisha ya kifamilia
Maendeleo endelevu - Kuanzisha ushirikiano wa kimataifa ambão utafanya kazi na kanisa mashinani katika kuleta maendeleo endelevu na yanayobadilisha hali za watu.
Taasisi ya mafunzo ya maaskofu - Kutumika kuandaa uongozi wa maaskofu watiifu na wenye ufanisi kote jumuiya ya Kianglikana
Kikosi kazi cha wanasheria - Kutatua masuala ya uhuru wa kanisa na wasiwasi wowote walionao wanasheria na wasajili wa kisheria wa Anglikana na kuendeleza malengo ya Tamko na Azimio la Jerusalem 
Ushirika wa waombaji - Kuhamasisha na kuendeleza mitandao ya waombezi wanaounganishwa kitaifa na kimataifa

Tuendapo kuihubiri injili ulimwenguni, tutakabiliana na mengi ambayo yatatuhitaji kutembea kwenye njia ya haki na rehema (Hosea 2:19; Mika 6:8). Tunatia nia ya kuhimizana kila mmoja kuwatia moyo wanaoteswa, sauti kwa wasionayo, utetezi kwa ajili ya wanaonyanyaswa, ulinzi kwa walio hatarini, hasa wanawake na watoto, kukirimu maskini, na kuendeleza kazi ya kutoa huduma bora za elimu na afya. Kama itakavyofaa, tunahimiza uundwaji wa mindandao mingine katika kushughulikia masuala haya.

ANGLIKANA YETU YA BAADAYE DUNIANI

Katika kuitangaza injili, ni lazima kwanza tuitetee injili dhidi ya matishio mbalimbali kutoka ndani na nje ya kanisa. Tunazikiri baraka za kipekee na ajabu za Mkutano huu, ambazo zinatuongoza katika kumwomba Mungu zaidi na zaidi, kwamba Jumuiya ya Waanglikana Duniani inaweza kuwa chombo chenye nguvu mikononi mwa Mungu kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Tunawaalika Waanglikana wote watiifu kutuunga mkono katika kazi hii njema ya kumtangaza Kristo kwa uaminifu kwa mataifa.

Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina
Waefeso 3:20-21

FAHARASA

Azimio la Lambeth I.10 - liliidhinishwa na Mkutano wa Lambeth wa mwaka 1998. http://www.anglicancommunion.org/resources/document-library/lambethconfe...

Baraza – hufanya kazi kama halmashauri ya kanisa

Baraza la Sinodi - linajumuisha Jopo la Washauri na Baraza la Maaskofu Wakuu wa Gafcon wanapokutana pamoja ili kutoa mapendekezo kwa ajili Mkutano wa Gafcon

Jopo la Washauri - linajumuisha askofu mmoja, mchungaji mmoja na mlei mmoja kutoka kila Jimbo la Gafcon na tawi la Gafcon, ambao wanatoa ushauri kwa Maaskofu Wakuu wa Gafcon.

Kikao cha Maaskofu Wakuu - Mkutano wa Maaskofu Wakuu wa Majimbo wanaoalikwa na Askofu Mkuu wa Canterbury

Maaskofu Wakuu wa Gafcon – Maaskofu Wakuu  ambao wameidhinisha Azimio la Yerusalemu na wamekubaliwa kuwa wajumbe wa Baraza la Maaskofu Wakuu wa Gafcon.

Majimbo ya Gafcon - Majimbo ambayo Nyumba ya Maaskofu au Sinodi ya Jimbo imeidhinisha Azimio la Yerusalemu na ambayo Askofu Mkuu wake ni Mjumbe wa Baraza la Maaskofu Wakuu wa Gafcon.

Matawi ya Gafcon - Tawi linaweza kuanzishwa kwa kutuma  maombi kwenye Baraza la Maaskofu Wakuu wa Gafcon kwa jimbo ambalo Askofu Mkuu wake sio mjumbe wa Baraza la Maaskofu Wakuu wa Gafcon.

Mihimili ya Jumuiya - Kuna Mihimili minne: Ofisi ya Askofu Mkuu wa Canterbury, Mkutano wa Lambeth, Kikao cha Maaskofu Wakuu na Halmashauri ya Ushauri ya Waanglikana Duniani.  http://www.anglicancommunion.org/structures/instruments-of-communion.aspx

Tamko la Kuala Lumpur - liliidhinishwa na Mtandao wa Waanglikana wa Nyanda za Kusini za Dunia mwaka 1997. http://www.globalsouthanglican.org/index.php/blog/comments/the_kuala_lum... nt_on_human_sexuality_2nd_encounter_in_the_south_10

Tamko na Azimio la Yerusalemu – Tamko lililokubaliwa na Mkutano ulioanzisha Gafcon mwaka 2008. . https://www.gafcon.org/resources/the-complete-jerusalem-statement

Sub Section: 

GAFCON Editorial Disclaimer

Keep informed of the latest news, updates and the different ways you can support Gafcon

Gafcon Secretariat, Christ Church Central, The DQ Centre, Fitzwilliam Street, Sheffield  S1 4JR  United Kingdom

[email protected]